Sunday, November 17, 2013
BABY ni neno la Kiingereza lenye maana ya
mtoto, tena mara nyingi linatumika kwa mtoto
mdogo. Pia lina maana nyingine ya mpenzi. Ni
neno maarufu sana siku hizi; hata wazee
kabisa, utasikia wanaitana baby!
Mbali na hilo, yapo maneno mengine kama
sweet, dear, honey na mengine mengi.
Maneno yote hayo ya Kiingereza, yana maana
zaidi ya moja, lakini kubwa zaidi ni
kumaanisha mpenzi, mpendwa (hutumika
katika kuonesha mapenzi ya dhati kwa
mwingine).
Leo nataka kukupa kitu kipya kabisa kichwani
mwako. Unahitaji utulivu wa hali ya juu ili
kujifunza hili. Ni maneno mazuri sana, ya
kipekee lakini kwa upande mwingine ni hatari
kwa sababu hukaribisha matatizo ambayo
hayakutarajiwa na mtumiaji.
HUTUMIKA WAPI HASA?
“Dear, naomba uniamshe saa 12:00 asubuhi,
kesho nina vikao vingi sana asubuhi,” inaweza
kuwa kauli ya mume akimwambia mkewe,
ambaye naye anamjibu: “Sawa sweet, usijali.”
Kwa hakika ndipo sehemu sahihi zaidi
kutumika. Ni maneno yenye mshawasha
mkubwa na huonesha penzi la dhati lililopo
moyoni mwa mhusika kwenda kwa mpenzi
wake.
Husisimua na kuongeza ladha ya mapenzi ya
kweli. Kumuita mpenzi wako kwa majina ya
kimapenzi huongeza zaidi upendo na msisimko
wa moyo. Mwenzi hujiona wa kipekee na
mapenzi huzidi kukua.
Kwa maana hiyo basi, ni sahihi zaidi kwa
wapenzi kuitana majina niliyotaja hapo juu na
mengine yanayofanana na hayo kwa lugha
yoyote ile, ila iwe inatambulika vizuri na
anayetamkiwa.
ATHARI SASA!
Kwa upande mwingine kuna athari za kutumia
maneno hayo. Zama hizi, maneno hayo
yanaonekana ya kawaida tu. Mtu yeyote
anaweza kumuita yeyote mpenzi, honey, baby
n.k. Hapo ndipo kwenye tatizo lenyewe.
Kwa ujumla wanawake ndiyo wanaongoza zaidi
kuitana majina hayo. Wakati mwingine huenda
mbali zaidi na kuwaita hata wanaume majina
hayo ya kimapenzi. Si rahisi kuona athari zake
kwa haraka na moja kwa moja, lakini zipo na
wengi zimewasababishia matatizo. Ngoja
tuone..
HUPUNGUZA THAMANI
Kama nilivyotangulia kusema awali, maneno
niliyotaja hapo juu husisimua na kuongeza
mapenzi. Kwa kuyatumia vinginevyo, basi kwa
kiasi kikubwa huanza kukuathiri na kupunguza
thamani ya neno lenyewe.
Kama unaweza kumwita mfanyakazi mwenzako
dear, mtu wa jinsi sawa na wewe sweet ni wazi
hata utakapomuita mpenzi wako au wewe
kuitwa na yeye, halitakuwa na nguvu sana ya
mapenzi kwa sababu ni neno ulilolizoea kila
wakati.
HUKARIBISHA USALITI
Wakati mwingine unaweza kujikuta umeingia
kwenye usaliti bila kutarajia. Veronica,
mfanyakazi wa saluni moja ya kiume iliyopo
Sinza, Dar alitoa ushuhuda ufuatao:
“Mimi naishi na mchumba wangu, tuna mtoto
mmoja mwenye miaka mitatu. Nafanya kazi
saluni. Tangu nimeanza hii kazi, nimejifunza
kutumia maneno matamu ya kumfurahisha
mteja na wakati mwingine kumfanya akupe
tipu baada ya kumaliza kazi.
“Kuna kaka mmoja nilizoeana naye sana. Kama
kawaida, huwa namkaribisha kwa kumuita
dear au sweet. Wakati nikiendelea kumfanyia
scrub, mazungumzo yetu hutawaliwa na dear,
sweet, nikajikuta nimezidi kumzoea.
“Kwa sababu tulibadilishana namba, mara
akaanza kuwa na mazoea ya kunitumia meseji,
akija ananipa pesa, anaondoka. Mazoea
yakazidi. Nikajikuta nimemzoea na kuna siku
ambayo siwezi kuisahau kabisa.
“Ni siku niliyomsaliti mchumba wangu...mbaya
zaidi na huyo jamaa naye ana mke wake.
Niliumia sana, lakini naamini kama
nisingekuwa na mazoea ya kumuita majina ya
kimapenzi nadhani nisingeingia mtegoni. Moyo
wangu unauma sana, najuta kumsaliti mpenzi
wangu.”
Unaweza usione athari hii moja kwa moja,
lakini ndugu zangu chukua jambo hili leo;
wanaume wengi wakiitwa kwa majina ya
kimapenzi husisimka sana – hujiona wenye
bahati na mara hushawishika kuingia mapenzi.
Kama mwanamke hatakuwa makini atajikuta
ametumbukia. Ya nini yote hayo, wakati
unaweza kubadilisha mazoea hayo?
ANGALIA TOFAUTI
Rafiki zangu, kati ya maneno niliyoyataja, kuna
ambayo yanakubalika kutumiwa na wasio na
uhusiano lakini wawe na undugu wa damu.
Mathalani baba, mama, kaka, dada, shangazi
nk.
Hakuna tatizo kumuita mtu mpendwa, lakini
siyo baby, sweet, mpenzi na mengine yenye
maana ya moja kwa moja ya kimapenzi.
Umenipata? Akili za kuambiwa, changanya na
zako kisha unazifanyia kazi! Chukua
kinachokufaa!
Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine. Wewe ni
muhimu sana kwangu. Bye!
Subscribe to:
Posts (Atom)